Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amepinga juhudi za wabunge kuharamisha siasa za “walala hai na walala hoi” zinazoendelezwa na naibu rais William Ruto.

Katika taarifa, Odinga amewasihi wabunge wamwache Ruto na wendani wake kuendelea na siasa zao pasipo kuwazuia akihoji kuwa kuwazuia itakuwa ni kuhujumu uhuru wa kujieleza ulioko kwenye katiba.

Na ili kukomesha siasa hizo, Odinga ametoa wito kwa viongozi wenye mtazamo tofauti kuwaelemisha Wakenya kuhusu athari za siasa kama hizo ili wawe macho.

Msimamo wa Odinga unajiri wakati ambapo kamati ya bunge la kitaifa kuhusu usalama chini ya uongozi wake mbunge wa Kiambaa Paul Koinange inataka siasa za hasla na dynasties zipigwe marufuku na zitajwe kama zinazoeneza chuki na uchochezi.