Shule ya Wasichana ya Moi Eldoret imefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia maandamano ya wanafunzi mapema hii leo kutaka mwalimu wao mkuu kutimuliwa.

Mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Uasin Gishu Gitonga Mbaka, amesema wanafunzi hao wana hadi kesho asubuhi kuondoka shuleni ili kuipa nafasi bodi ya shule hiyo kushughulikia matakwa yao.

Wanafunzi hao waliandamana mapema leo kushinikiza kuondolewa kwa mwalimu wao mkuu Christine Chumba ambaye wanamshtumu kwa kuwanyanyasa na kukosa kutilia manani masuala wanayoibua.

Juhudi za Mbaka kutuliza wanafunzi hao ziliambulia patupu baada yao kukataa kurejea darasani.