Washukiwa wawili kati ya watatu wamepatikana na hatia ya kupanga na kutekeleza shambulizi la kigaidi katika jumba la kibiashara la Westgate na kusababisha maafa ya watu 67.

Katika uamuzi wake, Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Francis Andayi amesema kuna ushahidi wa kutosha kudhibitisha kuwa Mohammed Abdi Ahmed na Hussein Hassan Mustafa walishirikiana kutekeleza tendo la ugaidi.

Hakimu Andayi hata hivyo amemuondolea mashtaka mshukiwa wa pili Liban Omar na kusema upande wa mashtaka haukutoa ushahidi wa kutosha kudhibitisha kuwa alikuwa miongoni mwa waliopanga na kutekeleza shambulizi hilo.

Hakimu Andayi amesema atawahukumu wawili hao Alhamisi tarehe 22 mwezi huu.

Kundi la kigaidi la Al Shabaab ambalo lina uhusiano na maharamia wa Al Qaeda lilidai kuhusika kwenye shambulizi hilo la tarehe 21 Septemba mwaka 2013.