Washukiwa kumi na sita wakiwemo wanasiasa na naibu chifu wanatazamiwa kufikishwa mahakamani hii leo baada yao kutiwa mbaroni kwa tuhuma za kuchochea mapigano ya kikabila katika eneo Marioshoni kaunti ya Nakuru.

WAtu watano wamefariki kutokana na mapigano hayo.

Kamishan wa eneo hilo George Natembeya anasema washukiwa hao watashtakiwa kwa makosa ya mauaji ya kukusudia, uchomaji wa nyumba, kuchangia vita na mashtaka mengine.

Natembeya anasema zaidi ya watu elfu tatu wametoroka makwao kutokana na mapigano hayo na kuongeza kuwa watu themanini na tatu wameumia tangu mapigano hayo kuzuka.

Mombasa

Wakati uo huo washukiwa wanne wanatazamiwa kufikishwa mahakamani hii leo kuhusiana na uvamizi katika eneo la Likoni kaunti ya Mombasa Ijumaa usiku.

Washukiwa hao wanatazamiwa kushtakiwa kwa kuwa wanachama wa kundi la kihalifu na kuwasababaishia watu majeraha.

Mbunge wa eneo hilo Mishi Mboko anasema visa hivyo vya uhalifu vinachangiwa na uuzaji wa mihadarati katika eneo hilo.